Polisi katika kisiwa cha Madeira, Ureno, wanaendelea na uchunguzi baada ya tukio la mtu mmoja kuchoma moto sanamu ya shaba ya nyota wa soka Cristiano Ronaldo, iliyopo nje ya Makumbusho ya CR7 jijini Funchal.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtuhumiwa anayejulikana mitandaoni kwa jina la zaino.tcc.filipe alirekodi video akimwaga kimiminika kwenye sanamu hilo, kisha kuwasha moto huku akicheza muziki wa rap.
Mtuhumiwa huyo alichapisha video hiyo kwenye mtandao wa Instagram akiwa ameambatanisha ujumbe wa kutisha uliomlenga Cristiano Ronaldo, ikiwemo kauli iliyosomeka: “Hii ni onyo la mwisho”.
Sanamu hilo lilizinduliwa rasmi mwaka 2014 na Cristiano Ronaldo mwenyewe, na si mara ya kwanza kulengwa na vitendo vya uharibifu.
Mamlaka za usalama zimesema tukio hilo linachukuliwa kwa uzito mkubwa, huku hatua za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Polisi wamewahakikishia wananchi kuwa wataendelea kulinda maeneo ya kihistoria na alama muhimu za utalii, huku wakisisitiza kuwa vitendo vya uharibifu na vitisho havitavumiliwa.


Post a Comment