Mchezaji wa soka raia wa Ureno mwenye asili ya Angola, Nassur Bacem, aliyekuwa akiitumikia klabu ya Lusitano Ginásio Clube Moncarapachense, amefariki dunia baada ya kupata mshtuko wa moyo na mfumo wa upumuaji (cardiorespiratory arrest) wakati wa mchezo wa Algarve Cup.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea tarehe 21 Januari 2026 mjini Olhão, wakati Moncarapachense ikiwania ushindi dhidi ya Imortal DC.
Bacem, aliyekuwa akicheza nafasi ya ulinzi, alianguka ghafla katikati ya mchezo baada ya kupatwa na tatizo hilo la kiafya.
Madaktari na wahudumu wa afya kutoka timu zote mbili walichukua hatua za haraka kujaribu kuokoa maisha yake, ikiwemo matumizi ya kifaa cha defibrillator, kabla ya kuwasili kwa gari la wagonjwa la huduma za dharura za Ureno (INEM).
Hata hivyo, licha ya juhudi zote hizo, Bacem alifariki dunia baadaye alipofikishwa hospitalini.
Kupitia taarifa rasmi, klabu ya Moncarapachense ilieleza kuwa Bacem “ameondoka mapema sana, akiacha pengo kubwa katika klabu na kwa wote waliomfahamu,” huku ikitoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wachezaji wenzake.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Ureno (FPF) pia limetoa salamu za rambirambi, na klabu mbalimbali alizowahi kuzitumikia mchezaji huyo, ikiwemo Sporting CP, zimemtaja Bacem kama mchezaji mwenye nidhamu, maadili mema na kujituma kwa kiwango cha juu.
Kufuatia msiba huo, Chama cha Soka cha Algarve kimetangaza kufuta shughuli na sherehe za maadhimisho ya miaka 104 ya kuanzishwa kwake, kama ishara ya heshima na maombolezo.
Nassur Bacem aliwahi kucheza katika akademi za Sporting CP na Braga, kabla ya kuitumikia klabu kadhaa za soka la kulipwa zikiwemo Leixões, MarÃtimo, Oliveira do Hospital, Camacha na hatimaye Moncarapachense.
Kifo cha Bacem kimeacha majonzi makubwa katika jamii ya soka nchini Ureno na kimetoa kumbusho la hatari za kiafya zinazoweza kujitokeza kwa wanamichezo, hata wale wenye umri mdogo na wanaoonekana kuwa na afya njema.



Post a Comment