Mchezaji wa zamani wa Real Madrid Wanawake, Kosovare Asllani, ametoa madai mazito kuhusu kile alichokiita mazingira yasiyo na afya na hatarishi kwa wachezaji wa kike ndani ya klabu hiyo.
Asllani amesema alipokuwa Real Madrid, alikumbana na utamaduni mbaya uliokuwa ukipuuzwa na uongozi, hali iliyomfanya hata kulazimishwa kucheza akiwa na majeraha, kinyume na ushauri wa wataalamu wa tiba.
“Kulikuwa na utamaduni usio na afya kwa wachezaji wa kike Real Madrid, na nami kwa namna fulani nilikuwa sehemu yake. Karibu walinilazimisha kucheza nikiwa nimeumia, bila msaada wowote. Uongozi haukufuata mapendekezo ya madaktari,” amesema Asllani.
Mshambuliaji huyo ameeleza kuwa uamuzi wa kuondoka klabuni haukuwa wa hiari bali ulilazimishwa na mazingira hayo, akisema alifanya hivyo ili kulinda taaluma yake na kuhakikisha anaendelea kucheza kwa muda mrefu zaidi.
“Kuondoka kwangu lilikuwa jambo la lazima ili kuilinda kazi yangu. Kwa bahati mbaya, Real Madrid kuna mazingira yasiyo salama na hatarishi kwa wachezaji wa kike,” ameongeza.
Licha ya madai hayo, Asllani amesema bado ana mapenzi makubwa kwa klabu hiyo, lakini anaamini iko mikononi mwa watu wasiowajali wachezaji kama binadamu.
“Ninaipenda Real Madrid sana, lakini naamini iko kwenye mikono mibaya. Kwao, wachezaji ni bidhaa tu, si binadamu. Haijalishi kama umeumia, unaonekana kama chombo cha kufikia malengo yao,” amesisitiza.
Kauli za Asllani zimeibua mjadala mpana kuhusu ustawi, haki na ulinzi wa wachezaji wa kike katika klabu kubwa za soka barani Ulaya, hususan katika soka la wanawake linaloendelea kukua kwa kasi.


Post a Comment