MOTSEPE "HAKUNA TIMU ITAKAYOPENDELEWA CAF"



Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amekanusha vikali madai yanayoenea kuhusu uwepo wa upendeleo kwa baadhi ya mataifa katika mashindano yanayoendeshwa na shirikisho hilo, akisisitiza kuwa hakuna nchi itakayopendelewa zaidi ya nyingine miongoni mwa wanachama 54 wa CAF.

Akizungumza na waandishi wa habari, Motsepe amesema alifanya mawasiliano ya moja kwa moja na marais wa nchi zote wanachama wa CAF, akiwahakikishia kuwa kanuni za haki, usawa na uwazi ndizo msingi wa uendeshaji wa mashindano yote ya soka barani Afrika.

“Nilikuwa naongea na marais wa nchi zote jana. Nikawaambia hakuna timu yoyote kati ya mataifa 54 wanachama wa CAF itatendewa tofauti na nchi nyingine. Hakuna timu itakayopendelewa kwenye mataifa yote 54 wanachama,” amesema Motsepe.

Kauli hiyo ya Rais wa CAF imekuja kufuatia malalamiko na mjadala mpana ulioibuka hivi karibuni, hususan katika michuano ya AFCON 2025, ambapo baadhi ya timu na wadau walieleza wasiwasi kuhusu masuala ya upangaji wa ratiba, viwanja, tiketi na usalama.

Motsepe amesisitiza kuwa CAF imejikita katika kulinda misingi ya fair play, akieleza kuwa shirikisho hilo litaendelea kuchukua hatua za haraka pale ambapo changamoto au malalamiko halali yatakapojitokeza.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post