Chama cha Jogging Wilaya ya Temeke (TEJA) kimetangaza kumalizika rasmi kwa mgogoro uliokuwa ukiikabili Dar Jogging Club, baada ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke (DAS) kutoa uamuzi kuhusu rufaa iliyowasilishwa na Club hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya TEJA iliyotolewa Januari 16, 2026 na kusambazwa kwa vilabu vyote vya jogging ndani na nje ya Wilaya ya Temeke, vikao vya pamoja vilifanyika vikihusisha Ofisi ya DAS, uongozi wa TEJA pamoja na Dar Jogging Club kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Dar Jogging Club ilikiri kukiuka kanuni kwa kugomea maelekezo yaliyotolewa na TEJA, jambo lililopelekea kuchukuliwa hatua za kinidhamu (ilifungiwa kushiriki matukio yote ya Jogging kuanzia tarehe 01 Mei hadi Novemba 30, 2025)
Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa, Club hiyo imeamriwa kulipa faini ya shilingi 50,000/= na imeruhusiwa kurejea kushiriki na kutekeleza majukumu yake katika tasnia ya Jogging kuaniza Januari 16, 2026.
Aidha, TEJA imeomba radhi kwa vilabu vyote vya jogging kwa changamoto au usumbufu wowote uliotokea wakati wa mchakato wa kusubiri uamuzi wa shauri hilo.
Chama hicho pia kimezitaka Club zote kuendelea kuzingatia kanuni, taratibu na maelekezo ya chama kwa lengo la kudumisha mshikamano, nidhamu na kukuza maendeleo ya mchezo wa Jogging ndani ya Wilaya ya Temeke.


Post a Comment