Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameonyesha uzalendo na mapenzi ya dhati kwa michezo kwa kugharamia kikamilifu matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya fainali ya marudiano ya Kombe la Shirikisho la CAF kati ya Simba SC na RS Berkane ya Morocco.
Fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumapili, tarehe 25 Mei 2025, saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Ragey Mohamed, Rais Mwinyi pia atahudhuria mchezo huo kama ishara ya mshikamano na kuunga mkono wawakilishi wa Tanzania katika soka la Afrika.
Katika hatua hiyo ya kipekee, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia itagharamia maandalizi yote muhimu ya uwanja kwa ajili ya mechi hiyo ya kihistoria. Hatua hii inalenga si tu kuiunga mkono Simba SC, bali pia kuendeleza maendeleo ya michezo nchini na kuimarisha hadhi ya Zanzibar katika ramani ya kimataifa ya michezo.
Maelfu ya mashabiki kutoka pande zote za Muungano wa Tanzania na mataifa mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo kubwa, linalotarajiwa kuwa na mvuto wa kipekee barani Afrika.

Post a Comment