UJUMBE MZITO KWA WANAOTAKA KUIFANYIA FIGISU SIMBA




Msemaji wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, ametuma ujumbe mzito kuelekea mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya RS Berkane, akisisitiza kuwa huu ni wakati wa Simba kutwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.


Ahmed Ally amesema kuwa Simba haitegemei historia wala uwanja maalum kupata ushindi, bali ubora wa kikosi cha sasa. “Simba tumeshafanya maajabu mengi sana, acha ya zamani. Msimu huu kila aliyetufunga, na sisi tumemfunga. Berkane ameshamaliza zamu yake, sasa ni zamu yetu,” amesema.


Akitambua umuhimu wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Ahmed aliongeza kuwa Simba inashinda si kwa sababu ya uwanja huo, bali kwa uwezo wa timu. “Uwanja wa Amaan ndio ulitupeleka fainali na sasa ndio utatupa ubingwa. Hatukukaliza deni na Hayati Rais Mwinyi, sasa tunakwenda kulipa mbele ya mtoto wake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi.”


Katika ujumbe wake wa tahadhari kwa wale wanaojaribu kuhujumu mafanikio ya Simba, Ahmed alisema wazi: “Tumevua kabisa vazi la utu na ustaarabu. Tumelivaa vazi la unyama. Hili ni jambo la heshima, hatutaki mzaha. Hatutamuonea mtu aibu, tutakuharibia kabisa.” 


Alihitimisha kwa kumkumbuka Hayati Dkt. John Magufuli ambaye alitabiri Simba kuwa klabu ya kwanza kutoka Tanzania kuleta ubingwa wa Afrika. “Makombe ya ndani tumeshashinda sana, lakini sasa tunalitaka hili kwa mara ya kwanza,” alisisitiza.


Fainali hiyo ya kihistoria inatarajiwa kuchezwa Jumapili, Mei 25, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.


 

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post