TUKIO LA TAULO KATIKA FAINALI YA AFCON GUMZO




Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) iliyochezwa mjini Rabat, Morocco, imeacha gumzo kubwa barani Afrika kufuatia matukio kadhaa ya utata yaliyojitokeza ndani na nje ya uwanja, licha ya Senegal kutwaa ubingwa kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco.

Miongoni mwa matukio yaliyoibua mjadala mkubwa ni kile kilichomkumba kipa wa akiba wa Senegal, Yehvann Diouf, ambaye aliripotiwa kusumbuliwa na waokota mipira pamoja na baadhi ya maafisa wa pembeni ya uwanja wakati wa mchezo huo, hususan katika kipindi cha muda wa nyongeza.

Kwa mujibu wa video zilizosambaa mitandaoni, Diouf alilazimika kulinda taulo la kipa namba moja wa Senegal, Édouard Mendy, ambayo ilikuwa ikiwekwa nyuma ya lango.



Taulo hiyo ilikuwa muhimu kwa kipa huyo kwa ajili ya kufuta mikono na glovu (jasho na unyevunyevu) mara kwa mara ili kudhibiti mpira vizuri.

Katika tukio lililozua taharuki, waokota mipira walionekana kujaribu kuondoa taulo hilo mara kwa mara, jambo lililomfanya Diouf kuingilia kati na kuilinda kwa nguvu. 

Kila alipohitajika, Diouf alimkabidhi Mendy taulo hiyo na kurejea kuilinda, hali iliyodhihirisha mshikamano na umakini mkubwa ndani ya kikosi cha Senegal.

Mbali na hilo, fainali hiyo iligubikwa na maamuzi tata ya waamuzi. Senegal walinyimwa bao katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili bila tukio hilo kutamwa kwenye VAR, kabla Morocco kupewa mkwaju wa penalti baada ya VAR kuhusika. 



Hatua hiyo ilisababisha wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani kwa muda kama ishara ya kupinga uamuzi huo, kabla ya kurejea kufuatia ushawishi wa nahodha wao, Sadio Mané.

Penalti ya nyota wa Morocco, Brahim Díaz, ilidakwa na Mendy, jambo lililoipa Senegal uhai mpya hadi kufunga bao la ushindi katika dakika ya nne ya muda wa ziada kupitia Pape Gueye.

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) linatarajiwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo, ikiwemo suala la wachezaji kuondoka uwanjani, vurugu za mashabiki na vitendo vya waokota mipira vinavyodaiwa kukiuka kanuni za mashindano.

Licha ya vurugu na utata uliotawala fainali hiyo, Senegal wamefanikiwa kutwaa ubingwa wao wa pili wa AFCON, huku tukio la Diouf na taulo likibaki kuwa moja ya picha zilizoakisi mshikamano na nidhamu ya kikosi hicho katika mazingira magumu.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post