SENEGAL WATOA MALALAMIKO KWA WALICHOFANYIWA KABLA YA FAINALI YA AFCON



Shirikisho la Soka la Senegal limetoa taarifa rasmi kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), likieleza wasiwasi wake kuhusu masuala kadhaa ya kiusalama, malazi na haki ya mashabiki wake nchini Morocco.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, timu ya taifa ya Senegal imedai kuwa ilikumbana na ukosefu wa ulinzi wa kutosha ilipowasili mjini Rabat, pamoja na malazi yasiyokidhi viwango vinavyotarajiwa kwa mashindano ya hadhi ya AFCON.

Baada ya kuwasilisha malalamiko rasmi, timu hiyo ilihamishiwa katika hoteli nyingine.



Aidha, Senegal imesema ilikataa kufanya mazoezi katika Kituo cha Kiufundi cha Morocco, ikieleza kuwa hadi sasa haijapata mrejesho wowote kuhusu maombi yao ya kupewa uwanja mbadala wa mazoezi.

Katika upande wa mashabiki, shirikisho hilo limebainisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa tiketi kwa mashabiki wa Senegal, huku likisema limepewa tiketi mbili tu za VVIP, bila fursa ya kununua tiketi za VIP au VVIP kama ilivyokuwa kwenye nusu fainali.


Pia limeeleza kuwa, licha ya kununua tiketi kwa ajili ya mashabiki wao, wamekumbana na vikwazo vikali kutoka CAF.

Kwa sasa, Senegal imepata tiketi 300 za Daraja la Pili (Category 2) pamoja na tiketi 1,700 za Daraja la Tatu (Category 3), idadi ambayo shirikisho hilo linaona haitoshi kwa wingi wa mashabiki wa Senegal waliopo Morocco.


Kutokana na hali hiyo, Senegal imetoa wito kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Ndani (LOC) kuchukua hatua za haraka kurekebisha changamoto hizo, ili kuhakikisha misingi ya haki, usawa, usalama na fair play inalindwa kwa maslahi ya mafanikio ya soka la Afrika.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post