Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amelaani vikali kile alichokiita “matukio yasiyokubalika” yaliotokea katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), baada ya baadhi ya wachezaji wa Senegal pamoja na benchi la ufundi kuondoka uwanjani kupinga penati waliopewa Morocco.
Kupitia taarifa yake katika ukurasa wake wa Instagram, Infantino amesema kuwa “Tunalaani vikali tabia za baadhi ya mashabiki pamoja na baadhi ya wachezaji na benchi la ufundi la Senegal. Haikubaliki kabisa kuondoka uwanjani”
Aliongeza kuwa vitendo vya vurugu pia havina nafasi katika mpira wa miguu “Ni jambo lisilokubalika kuondoka uwanjani kwa, na hivyo hivyo, vurugu hazikubaliki katika mchezo wetu.”
Fainali hiyo iligubikwa na sintofahamu baada ya wachezaji wengi wa Senegal kuondoka uwanjani dakika za lala salama, wakati matokeo yakiwa 0-0, kufuatia uamuzi wa VAR uliohipatia Morocco penati baada ya Brahim DÃaz kuangushwa.
Mchezaji, Sadio Mané, alibaki uwanjani na kuwasihi wenzake warudi ili mchezo uendelee. Hasira za Senegal ziliongezeka baada ya bao lao kukataliwa dakika chache kabla kwa kile kilichoonekana kama faulo.
Wakati huohuo, vurugu zililipuka jukwaani ambapo baadhi ya mashabiki wa Senegal walijaribu kuingia uwanjani na kupambana na maafisa wa usalama.
Mchezo ulisimamishwa kwa takribani dakika 20 kabla ya Brahim DÃaz kupiga penati, ambayo aliipiga ambayo ilidakwa na kipa wa Senegal, Édouard Mendy.
Baadaye, Pape Gueye alifunga bao la ushindi katika dakika ya nne ya muda wa ziada na kuipa Senegal ushindi wa 1-0 na ubingwa wa AFCON.
Infantino pia aliipongeza Morocco kwa mashindano mazuri na kwa kuwa waandaaji bora, jambo linalowapa hamasa kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia la 2030 watakaloshiriki kuandaa.
“Ni lazima tuheshimu maamuzi ya waamuzi wa mechi ndani na nje ya uwanja. Timu lazima zishindane uwanjani kwa kuzingatia sheria za mchezo, kwani jambo lolote tofauti linaweka hatarini misingi ya mpira wa miguu,” alisema.
Infantino alisisitiza kuwa matukio kama hayo yanatuma ujumbe mbaya kwa mashabiki duniani kote na hayapaswi kurudiwa tena, akitarajia Kamati ya Nidhamu ya CAF kuchukua hatua stahiki.




Post a Comment