DAR JOGGING CLUB YAPINGA TAARIFA YA TEJA, YASEMA HAIJAWAHI KUKIRI KOSA WALA KULIPA FAINI




Uongozi wa Dar Jogging Club umeeleza kusikitishwa na kushangazwa na taarifa inayosambaa mitandaoni na Chama cha Jogging Wilaya ya Temeke (TEJA) na kusainiwa na Mwenyekiti wake, Rashid Pazzi Mvogogo, ikidai kuwepo kwa hukumu iliyotolewa dhidi ya Club hiyo kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke.

Kupitia taarifa rasmi, Dar Jogging Club imesema kuwa tayari ilikuwa imekata rufaa kupinga hatua zilizochukuliwa awali, hivyo inashangazwa, kutolewa kwa taarifa ya hukumu bila Club hiyo kushirikishwa, kusikilizwa wala kupewa nafasi ya kujitetea, hali ambayo ni kinyume na misingi ya haki na taratibu za uendeshaji wa michezo.

Uongozi wa Club hiyo umeeleza kuwa haujawahi kukiri kosa lolote, kuomba msamaha wala kukubali kulipa faini yoyote kama inavyodaiwa kwenye taarifa ya TEJA.




Aidha, umesisitiza kuwa madai hayo ni ya kupotosha na yanaonekana kulenga kuchafua taswira ya Club yao pamoja na viongozi wake, wakati juhudi za kutafuta suluhu ya haki kupitia mamlaka husika zilikuwa zinaendelea kwa njia ya mazungumzo na rufaa.

Dar Jogging Club imeeleza masikitiko yake kuona taarifa hiyo ikikiuka maelewano ya awali na kupuuza mchakato wa rufaa uliokuwa unaendelea, jambo linaloibua mashaka juu ya uhalali wa maamuzi yanayodaiwa kutolewa.

Katika hitimisho lake, uongozi wa Dar Jogging Club umewataka wanachama na wadau wake kuendelea kuwa watulivu, huku ukisisitiza kuwa Club itaendelea kusimamia misingi ya haki, uadilifu na kufuata sheria na miongozo ya michezo nchini, ikiahidi kulishughulikia suala hilo kupitia vyombo vya juu vya maamuzi.


Taarifa ya Chama cha Jogging Wilaya ya Temeke (TEJA)

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post