Uongozi wa klabu ya Junguni United umechukua hatua kali kwa kuwasimamisha na kuwafukuza wachezaji wake saba waliobainika kujihusisha na kubeti (kubashiri matokeo ya michezo), kinyume na kanuni za mchezo wa soka Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa tarehe 24 Aprili 2025 na Katibu wa klabu hiyo, Suleiman Mwidani, imewataja wachezaji waliochukuliwa hatua kuwa ni: Salum Athumani Chubi (Chubi), Ramadhan Ally Omar (Matuidi), Abdallah Sebastian Ponera, Danford Mosses Kaswa, Bakar Athumani Jomba (Jomba Jomba), Rashid Abdallah Njete pamoja na Iddi Said Korongo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wachezaji hao walijihusisha na ubashiri wa matokeo katika michezo miwili ya klabu hiyo dhidi ya Malindi na New City. Kitendo hicho kinatajwa kuwa kinyume na katiba ya klabu na pia kinakiuka kanuni za Ligi Kuu ya Zanzibar kwa msimu wa 2024/2025, hususan sura ya 23, kifungu cha 2 na 3.
"Baada ya uchunguzi wa kina kufanyika, tumebaini kuwa wachezaji hawa walikiuka sheria kwa kujihusisha na mchezo wa kubeti. Kwa msingi huo, tumeamua kuwasimamisha na kuwafukuza rasmi kutoka klabuni, pamoja na kuwazuia kushiriki shughuli yoyote ndani ya klabu yetu," imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, klabu hiyo imetoa wito kwa Shirikisho la Soka Zanzibar kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wachezaji hao ili kukomesha kabisa tabia ya kubashiri michezo, ambayo inaelezwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo ya soka visiwani humo.

Post a Comment