Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza kuwa Zanzibar itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Mabingwa wa Shule za Afrika mwaka 2024.
Michuano hiyo inayofanyia kwa msimu wa pili itaanza Mei 21 hadi Mei 24 katika Uwanja wa Amaan Complex, visiwani humo.
Michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya vijana inayohusisha mabingwa kutoka kwenye kanda mbalimbali Afrika itavutia ugeni mkubwa Zanzibar, visiwa vinavyofahamika zaidi kwa utalii duniani.
Kwa msimu wa pili, ushiriki tangu ngazi za awali umekuwa mkubwa, ukiwa na ongezeko la asilimia 40 la washiriki kutoka shule 28,862 zilizopo kwenye nchi 44 barani Afrika.
Fainali hizo zitahudhuriwa pia na malejendari wa soka Afrika, ili kutoa hamasa na kuwa chachu kwa washiriki, ikiwa ni jukwaa linalotumika pia kukuza vipaji kwa wavulana na wasichana Afrika.
Kila mshindi kwa wavulana na wasichana atapewa zawadi ya USD 300,000 (shilingi milioni 777), mshindi wa pili akipewa USD 200,000 na mshindi wa tatu USD 150,000.
Mwaka jana CS Ben Sekou Sylla toka Guinea na Fountain Gate School ya Tanzania ziliibuka mabingwa kwa wavulana na wasichana mtawalia, katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini.

Post a Comment